Mjane wa Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Maria Nyerere amepokea nishani ya heshima kutoka Jamhuri ya Angola ya kutambua mchango wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika harakati za ukombozi na upatikanaji wa amani nchini Angola.
Akikabidhi nishani hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amesema kuwa Nishani hiyo ni heshima kubwa kwa Mwalimu Nyerere na Tanzania kwa ujumla ambayo alieleza kuwa inatokana na mchango wa Mwalimu Nyerere kwenye harakati za ukombozi wa Angola. Aliongeza kuwa ardhi ya Tanzania ilitumika kwa ajili ya kutoa hifadhi, kuandaa mipango na mikakati pamoja na mafunzo kwa wapigania uhuru wa mataifa mbalimbali, ikiwemo Angola.
Naye Balozi wa Angola nchini, Mhe. Domingos de Almeida da Silva Coelho aliyeungana na Mhe. Kombo kuikabidhi nishani hiyo kwa Mjane wa Baba wa Taifa alisema “Angola inatambua mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika harakati za uhuru wake. Nishani hii ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru wa Angola na uthibitisho wa mshikamano wa kweli wa Afrika.”
Kwa upande wake Mama Maria Nyerere ameishukuru Angola kwa nishani hiyo kubwa ya heshima kama alama ya kutambua mchango wa Hayati mumewe akiongeza kuwa juhudi na jitihada za Mwalimu Nyerere za za kuikomboa Afrika zisingezaa matunda bila ushirikiano na mshikamano alioupata Mwalimu Nyerere kutoka kwa viongozi wenzake wengine wa Afrika.
Akishukuru kwa niaba ya familia, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere amesema Mwalimu Nyerere aliona Tanzania haipo huru hadi nchi zingine za Afrika zitakapokuwa huru hivyo aliamua kusaidia na wengine. “Tunashukuru kwa heshima hii kubwa na hata tunapokuja nchini kwenu mnatupokea kwa heshima kubwa tunashukuru sana.”
Mwalimu Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kuanzia 1964 hadi 1985. Nchi nyingine zilizonufaika na jitihada hizo ni pamoja na Namibia, Msumbiji, Afrika Kusini, Zimbabwe, Guinea-Bissau na Cape Verde.
